(MICHEZO>>)WASICHANA WATOANA JASHO AIRTEL RISING STARS

WASICHANA WATOANA JASHO AIRTEL RISING STARS



Mchezaji timu ya soka ya wasichana ya Ilala Fatuma Salumu (Kushoto) akichuana na mchezaji wa timu ya Simba Queens Mwanaidi Hamisi katika michuano ya Airtel Rising Stars kwenye kiwanja cha kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam jana. Simba Queens walishinda 2 – 0.

Mchezaji timu ya soka ya wasichana ya Ilala Fatuma Salumu (Kushoto) akiwania mpira na mchezaji wa timu ya Simba Queens Asha Abdul katika michuano ya Airtel Rising Stars kwenye kiwanja cha kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam jana. Simba Queens walishinda 2 – 0.

Mchezaji timu ya soka ya wasichana ya Simba Queens Eva Charles (Kushoto) akimtoka mchezaji wa timu ya Ilala Fatuma Salumu katika michuano ya Airtel Rising Stars kwenye kiwanja cha kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam jana. Simba Queens walishinda 2 – 0

Timu ya wasichana ya Simba Queens jana iliibuka na ushindi wa 2 – 0 dhidi ya timu ya Ilala katika michuano ya vijana ya U-17 ya Airtel Rising Stars kwa mkoa wa kisoka wa Ilala. Mchezo huo ulipigwa katika uwanja wa kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam jana.
Timu zilianza mchezo huo kwa kujihami na kushambuliana kwa kushtukiza. Simba Queens walifanikiwa kupata goli la mapema baada ya Zainab Mahmoud kuifungia timu yake katika dakika ya tano.
Timu ya Ilala ilibadilika baada ya kuwa nyuma kwa goli moja na kuanza kushambulia kwa kasi. Lakini juhuhudi hizo hazikuzaa matunda na hadi mapumziko timu ya Simba Queens walikua wanaongoza kwa goli moja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu zote zikicheza kwa umakini wa hali ya juu. Simba Queens waliongeza kasi na kufanikiwa kupata goli la pili katika dakika ya 46 kupitia kwa Khadija Ally baada ya kuachia shuti kali lililotinga wavuni moja kwa moja.
Katika kiwanja cha Tanganyika Packers, Mburahati Queens iliichakaza Lulu Queens kwa magoli 2 -1. Wafungaji wa Mburahati Queens walikua ni Anne Adrea dakika ya 56 na Janeth Christopher dakika ya 90. Wakati kwa upande wa Lulu walipata goli lao kupitia kwaOpah Clement dakika ya 46.
Katika kiwanja cha Makangarawe Yombo Timu ya wavulana ya Wakati Ujao ilipata ushindi wa 2 -1 dhidi ya Dubu. Kwa upande wa wasichana timu za Evergreen Queens na Temeke Queens zilienda sare ya bila kufungana.
Michuano hii ya vijana ambayo kwa jiji la Dar es Salaam imeshaanza kwa takriban katika mikoa yake yote ya kimichezo, inafuatiliwa kwa karibu na jopo la makocha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) bila kusahau timu mbalimbali ambazo zinawanyatia kwa karibu vijana wenye vipaji kutoka michuano hiyo.
Huu ni mwaka wa tano kwa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kuanzisha na kudhamini michuano hiyo ya Airtel Rising Stars yenye lengo la kutafuta na kuendeleza vipaji.
Mashindano ya Airtel Rising Stars mwaka huu yanajumuisha mikoa ya Ilala, Temeke, Kinondoni, Morogoro, Mbeya, Mwanza na Arusha ambapo fainali za taifa za michezo hiyo zimepagwa kupigwa jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 11 hadi 21.